John 6

Isa Alisha Wanaume 5,000

(Mathayo 14:13-21; Marko 6:30-44; Luka 9:10-17)

1 aBaada ya haya, Isa alikwenda ng’ambo ya Bahari ya Galilaya, ambayo pia huitwa Bahari ya Tiberia. 2 bUmati mkubwa wa watu uliendelea kumfuata, kwa sababu waliona ishara nyingi za miujiza alizofanya kwa wagonjwa. 3 cKisha Isa akapanda mlimani akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. 4 dPasaka ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.

5 eIsa alipotazama na kuuona ule umati mkubwa wa watu ukimjia, akamwambia Filipo, “Tutanunua wapi mikate ili watu hawa wale?” 6Aliuliza swali hili kumpima, kwa maana alishajua la kufanya.

7 fFilipo akamjibu, “Hata fedha kiasi cha dinari mia mbili,
Dinari 200 ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku 200; mshahara wa kibarua ulikuwa dinari moja kwa siku.
hazitoshi kununua mikate ya kuwapa watu hawa ili kila mtu apate kidogo.”

8 hMmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, ndugu yake Simoni Petro, akamwambia, 9 i“Hapa kuna mvulana mmoja mwenye mikate mitano ya shayiri na samaki wawili wadogo. Lakini hivi vitatosha nini kwa umati huu wote?”

10Isa akasema, “Waketisheni watu chini.” Palikuwa na majani mengi katika eneo lile, nao watu wakaketi. Palikuwa na wanaume wapatao 5,000. 11 jNdipo Isa akachukua ile mikate, akamshukuru Mungu na kuwagawia wale watu waliokuwa wameketi. Akafanya vivyo hivyo na wale samaki. Kila mtu akapata kadiri alivyotaka.

12Watu wote walipokwisha kula na kushiba, akawaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki vya ile mikate, kisipotee chochote.” 13Hivyo wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili kwa vipande vya ile mikate mitano ya shayiri na samaki wale wawili wadogo vilivyobakishwa na waliokula.

14 kBaada ya watu kuona muujiza ule Isa aliofanya, walianza kusema, “Hakika huyu ndiye Nabii ajaye ulimwenguni!” 15 lIsa akijua kwamba walitaka kuja kumfanya awe mfalme wao, kwa nguvu, akajitenga nao akaenda milimani peke yake.

Isa Atembea Juu Ya Maji

(Mathayo 14:22-33; Marko 6:45-52)

16 mIlipofika jioni, wanafunzi wake waliteremka kwenda baharini. 17Wakaingia kwenye mashua, wakaanza kuvuka bahari kwenda Kapernaumu. Wakati huu kulikuwa tayari giza na Isa alikuwa hajajumuika nao. 18Bahari ikachafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma. 19 nWanafunzi walipokuwa wamekwenda mwendo wa karibu maili tatu au nne,
Maili tatu au nne ni kama kilomita 5 au 6.
walimwona Isa akitembea juu ya maji akikaribia mashua, nao wakaogopa sana.
20 pLakini Isa akawaambia, “Ni mimi. Msiogope.” 21Ndipo wakamkaribisha kwa furaha ndani ya mashua, na mara wakafika ufuoni walikokuwa wakienda.

Watu Wanamtafuta Isa

22 qSiku iliyofuata, wale watu waliokuwa wamebaki ng’ambo waliona kwamba palikuwepo na mashua moja tu na kwamba Isa hakuwa ameondoka pamoja na wanafunzi wake, ila walikuwa wameondoka peke yao. 23 rLakini zikaja mashua nyingine kutoka Tiberia zikafika karibu na mahali pale walipokula mikate baada ya Bwana kumshukuru Mungu. 24Mara wale watu wakatambua kwamba Isa hakuwepo hapo, wala wanafunzi wake. Wakaingia kwenye mashua hizo, wakaenda Kapernaumu ili kumtafuta Isa.

Isa Ni Mkate Wa Uzima

25 sWalipomkuta Isa ng’ambo ya bahari wakamuuliza, “Rabi, umefika lini huku?”

26 tIsa akawajibu, “Amin, amin nawaambia, ninyi hamnitafuti kwa kuwa mliona ishara na miujiza, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. 27 uMsishughulikie chakula kiharibikacho, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele, ambacho Mwana wa Adamu atawapa. Yeye ndiye ambaye Mungu Baba amemtia muhuri.”

28Ndipo wakamuuliza, “Tufanye nini ili tupate kuitenda kazi ya Mungu?”

29 vIsa akawajibu, “Kazi ya Mungu ndiyo hii: Mwaminini yeye aliyetumwa naye.”

30 wHivyo wakamuuliza, “Utafanya ishara gani ya muujiza, ili tuione tukuamini? Utafanya jambo gani? 31 xBaba zetu walikula mana jangwani, kama ilivyoandikwa, ‘Aliwapa mikate kutoka mbinguni ili wale.’ ”

32 yIsa akawaambia, “Amin, amin nawaambia, si Musa aliyewapa mikate kutoka mbinguni, bali Baba yangu ndiye anawapa mkate wa kweli kutoka mbinguni. 33 zKwa maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.”

34 aaWakamwambia, “Bwana, kuanzia sasa tupatie huo mkate siku zote.”

35 abIsa akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uzima. Yeye ajaye kwangu, hataona njaa kamwe na yeye aniaminiye, hataona kiu kamwe. 36 acLakini kama nilivyowaambia, mmeniona lakini bado hamwamini. 37 adWale wote anipao Baba watakuja kwangu na yeyote ajaye kwangu, sitamfukuzia nje kamwe. 38 aeKwa kuwa nimeshuka kutoka mbinguni si ili kufanya mapenzi yangu, bali mapenzi yake yeye aliyenituma. 39 afHaya ndiyo mapenzi yake yeye aliyenituma, kwamba, nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa, bali niwafufue siku ya mwisho. 40 agKwa maana mapenzi ya Baba yangu ni kwamba kila mmoja amtazamaye, Mwana na kumwamini awe na uzima wa milele, nami nitawafufua siku ya mwisho.”

41Wayahudi wakaanza kunung’unika kwa kuwa alisema, “Mimi ndimi mkate ulioshuka kutoka mbinguni.” 42 ahWakasema, “Huyu si Isa, mwana wa Yusufu, ambaye baba yake na mama yake tunawajua? Anawezaje basi sasa kusema, ‘Nimeshuka kutoka mbinguni’?”

43Hivyo Isa akawaambia, “Acheni kunung’unikiana ninyi kwa ninyi. 44Hakuna mtu awezaye kuja kwangu kama asipovutwa na Baba aliyenituma, nami nitamfufua siku ya mwisho. 45 aiImeandikwa katika Manabii, ‘Wote watafundishwa na Mungu.’ Yeyote amsikilizaye Baba na kujifunza kutoka kwake, huyo huja kwangu. 46 ajHakuna mtu yeyote aliyemwona Baba isipokuwa yeye atokaye kwa Mungu, yeye ndiye peke yake aliyemwona Baba. 47 akAmin, amin nawaambia, yeye anayeamini anao uzima wa milele. 48 alMimi ni mkate wa uzima. 49 amBaba zenu walikula mana jangwani, lakini wakafa. 50 anLakini hapa kuna mkate utokao mbinguni, ambao mtu yeyote akiula, hatakufa. 51 aoMimi ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni. Mtu yeyote akiula mkate huu, ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu, ambao nitautoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.”

52 apNdipo Wayahudi wakaanza kuhojiana vikali wao kwa wao wakisema, “Mtu huyu awezaje kutupatia mwili wake tuule?”

53 aqHivyo Isa akawaambia, “Amin, amin nawaambia, msipoula mwili wa Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. 54 arMtu yeyote aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu, anao uzima wa milele. Nami nitamfufua siku ya mwisho. 55Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli na damu yangu ni kinywaji cha kweli. 56 asYeyote alaye mwili wangu na kunywa damu yangu, atakaa ndani yangu nami nitakaa ndani yake. 57 atKama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, na kama nami ninavyoishi kwa sababu ya Baba, hivyo anilaye mimi ataishi kwa sababu yangu. 58 auHuu ndio mkate ushukao kutoka mbinguni, si kama ule mkate baba zenu waliokula nao wakafa. Lakini yeye aulaye mkate huu ataishi milele.” 59Isa alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika sinagogi huko Kapernaumu.

Wafuasi Wengi Wamwacha Isa

60 avWengi wa wafuasi wake waliposikia jambo hili wakasema, “Mafundisho haya ni magumu. Ni nani awezaye kuyapokea?”

61 awIsa alipojua kwamba wafuasi wake wananung’unika kuhusu mafundisho yake, akawaambia, “Je, jambo hili limewaudhi? 62 axIngekuwaje basi kama mngemwona Mwana wa Adamu akipaa kwenda zake huko alipokuwa kwanza? 63 ayRoho ndiye atiaye uzima, mwili haufai kitu. Maneno haya niliyowaambia ni Roho tena ni uzima. 64 azLakini baadhi yenu hamwamini.” Kwa maana Isa alifahamu tangu mwanzo wale ambao hawangemwamini miongoni mwao na yule ambaye angemsaliti. 65 baAkaendelea kusema, “Hii ndiyo sababu niliwaambia kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.”

66 bbTangu wakati huo wafuasi wake wengi wakarejea nyuma wakaacha kumfuata.

67 bcHivyo Isa akawauliza wale wanafunzi wake kumi na wawili, “Je, ninyi pia mnataka kuondoka?”

68 bdSimoni Petro akamjibu, “Bwana, tuondoke twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. 69 beTunaamini na kujua kuwa wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu.”

70 bfNdipo Isa akajibu, “Je, sikuwachagua ninyi kumi na wawili? Lakini mmoja wenu ni ibilisi.” 71 bg(Hapa alikuwa anasema juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Ingawa alikuwa mmoja wa wale kumi na wawili, ndiye ambaye baadaye angemsaliti Isa.)
Copyright information for SwhKC